KAMPUNI YA STARMEDIA(STARTIMES)IMETOA MISAADA

Meneja wa Mauzo wa Kampuni ya Startime David Kisaka (kushoto)akikabidhi vifaa hivyo kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi:Anna Mang’enya(kulia)pembeni ni wanafunzi wa shule hiyo wenye ulemavu wasiona na kusikia.


KAMPUNI ya Starmedia(Startimes) imetoa misaada mbalimbali ikiwemo vyakula kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko vyenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 3.

Akikabidhi msaada huo, Meneja wa Mauzo wa Kampuni hiyo David Kisaka alisema msaada uliolenga kutambua umuhimu wa jamii katika huduma wanazozitoa,utawasaidia wanafunzi hao kwa namna moja au nyingine wakiwa shuleni hapo.

Alisema msaada huo vikiwemo vitabu penseli,sabuni, na vinginevyo ni muendelezo wao katika kuisaidia jamii inayowazunguka huku akisisitiza kuwa malengo ya kampuni hiyo ni kuhakikisha wanasaidia na Serikali kutatua baadhi ya changamoto inayokabiliana nazo.

“Ukiacha msaada huu, tayari tumeshatoa msaada mwingine ikiwemo televisheni iliyounganishwa na king’amuzi chenye muda wa matangazo kwa mwaka mzima katika Hospitali ya Mwananyamala, hii yote ni kuonyesha namna gani tunavyofanya kazi pamoja na jamii ”

Aidha alisema huu ni mwanzo kwani tayari kampuni hiyo imeweka mipango madhubuti ya kuhakikisha inashirikiana kikamilifu na jamii kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Anna Mang’enya, mbali na kushukuru kwa msaada huo pia ameyaomba makampuni mengine kujitokeza na kuwapa msaada ili kuwawezesha kukabiliana na matatizo mbalimbali yalilyopo shuleni hapo.

Alisema Shule hiyo inayowahudumia watoto wa aina mbalimbali wakiwemo wenye ulemavu, wanahitaji msaada wa vyakula, vitabu pamoja na vifaa mbalimbali vinavyowasaidia kuwajengea uelewa wa masomo.

http://www.fullshangweblog.com/2013/02/01/kampuni-ya-starmediastartimesimetoa-misaada/

No comments:

Post a Comment